Andrew Komba

Kutumia Simu Au Kompyuta Kwa Muda Mrefu Ni Mbaya Sana Kwako

Kutumia-Simu-Au-Kompyuta-Kwa-Muda-Mrefu-Ni-Mbaya-Sana-Kwako


Hakuna asiyefahamu madhara yanayoweza sababishwa na matumizi ya kompyuta au simu kwa muda mrefu lakini wengi wetu tumekuwa tukipuuza na kuendelea kutumia vifaa hivyo kwani vimekuwa kama sehemu ya maisha yetu, kwa sababu kupitia vifaa hivyo kama tv na simu tunaweza kupata habari mbali mbali kwa urahisi huku kompyuta zikitusaidia kufanya shughuli zetu za kiofisi, na kuna baadhi ya watu wanalazimika kutumia kompyuta kwa siku nzima kutokana na shughuli zao kuwataka kufanya hivyo ili kujitengenezea kipato huku vijana siku hizi simu za mkononi ndiyo imekuwa sehemu ya maisha yetu kwani hatuwezi kukaa hata dakika kadhaa pasipo kuangalia nini kimetokea kwenye ulimwengu wa mitandao.

Ukweli ni kwamba kama unaangalia kompyuta, simu, tv, au chombo kingine chochote cha kielektroniki chenye skrini kwa zaidi ya masaa saba kwa siku, basi tambua lazima utakuja kuwa na matatizo ya macho huko uzeeni kwako. Sasa hapo unaweza ukasema kwamba ni ule mwanga unaotoka kwenye vifaa hivyo ndiyo tatizo kubwa lakini si kweli tatizo ni machozi yaliyokuwa kwenye macho.

Machozi kivipi.

Machozi yanakazi kubwa sana kwenye macho na sote tunayapenda machozi ukiachilia mbali katika kuonesha hisia za mtu, ila machozi kwenye macho yanakazi kubwa sana, kama kuhakikisha macho yetu yana kuwa masafi muda wote pamoja na kuyalainisha. Sehemu muhimu katika mfumo wa machozi ni kope za macho. Pindi mlija wa machozi unaofahamika kitaalamu kama Nasolacrimal Duct au Tear Duct ukiwa unahifadhi machozi kwenye kingo za macho yetu, machozi hayo hujaa. Hivyo kama tukikopesa macho, tunasaidia kusambaza machozi hayo katika jicho zima na kusaidia kuliweka jicho katika hali ya usafi, yaani ni kama windshield inavyosafisha kioo cha gari.

Sasa, kivipi hii inahusiana na kuangalia kompyuta, tv, au simu kwa muda mrefu.

Unapokuwa unaangalia kompyuta, simu, au tv kwa muda mrefu macho huwa yanakopesa kwa muda mchache sana, pamoja na kutanuka kuliko kawaida na hii inasababisha machozi yanayolainisha jicho kukauka haraka sana kutokana na kukodoa kwa muda mrefu, hivyo hupelekea mtu kupata ugonjwa wa kukauka macho Dry Eye Sydrome.

Hivyo basi, kama unajua ni vigumu kwako kukaa mbali na kompyuta, simu, au tv unaweza ukafanya mambo haya yafuatayo ili kuokoa macho yako:

  • Hakikisha unapumzika kutumia kifaa chako (Simu, kompyuta, au tv) walau kila baada ya dakika 30
  • Hakikisha skrini inakuwa chini yako, yaani uwe unaangalia kwa chini, hii itasababisha macho yako yawe yanakopesa kidogo.
  • Epuka kukaa sehemu ambazo hewa inapuliza kwa kasi, kama chini ya AC au karibu na feni
  • Hakikisha eneo ulipo kuna hewa ya uvuguvugu kidogo

Tuandikie maoni yako kuhusu chapisho hili kwenye ukurasa wetu wa Facebook, pia usisahau kusubscribe channel yetu ya YouTube kwa video zilizochambuliwa kwa undani zaidi juu ya masuala yanayotokea Duniani.

INAYOTAZAMWA SASA: KITU ALICHOFANYA MWANAMITINDO HUYU SIO CHA KAWAIDA